Vyama vinne vilivyounda Ukawa, Chadema, CUF,
NCCR-Mageuzi na NLD, vimekubaliana kusimamisha mgombea mmoja wa kuanzia
ngazi ya urais, lakini kila chama kitateua mgombea wake kabla ya
kukubaliana mtu atakayeungwa mkono na vyama vyote.
Ratiba iliyotolewa jana na Chadema inaonyesha
kuwa chama hicho kitatumia siku 76, kuanzia Mei 18, kumaliza mchakato
wa kuwapata wagombea wake wa nafasi za udiwani, ubunge na urais kwa
kuhitimisha na Mkutano Mkuu. Kwa mujibu wa ratiba hiyo, Chadema itampata
mgombea wake wa urais takriban siku 14 zaidi kulinganisha na mwaka 2010
wakati Dk Willibrod Slaa alipoteuliwa.
Kwa mujibu wa Ibara ya 7.710 (C) ya katiba ya
Chadema, Mkutano Mkuu ndiyo chombo chenye mamlaka ya kumpitisha mgombea
wa urais kwa tiketi ya chama hicho.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe aliwaambia
wanahabari jana kuwa kamati hiyo imeridhia mchakato wa uchukuaji na
urejeshaji fomu uanze ili watia nia katika maeneo mbalimbali waanze
kuchukua fomu za udiwani, uwakilishi na ubunge.
Katika ratiba hiyo , chama hicho kimeyapa
kipaumbele maeneo yanayoonekana kutokuwa na madiwani na wabunge, kuanza
kuchukua fomu siku ya kwanza ya kazi hiyo na kuzirudisha Juni 25.
Aidha ratiba hiyo inaonyesha kuwa makada waliopo
kwenye maeneo yenye madiwani watachukua na kurejesha fomu ndani ya siku
10 kuanzia Julai Mosi.
Wakati huo, maeneo yenye wabunge kwa sasa
yakipatiwa siku tano za kukamilisha uchukuaji na urejeshaji wa fomu hizo
kuanzia Julai 6 hadi 10 huku vigogo wanaounyemelea urais wakipigiwa
kipenga Julai 20 hadi 25.
Mara baada ya wagombea urais kukamilisha taratibu
za kinyang’anyiro, Chadema imepanga kufanya uteuzi wa mwisho wa wagombea
ubunge Agosti 1 na 2 huku Baraza Kuu likipangwa kukutana siku
inayofuata kabla ya Mkutano Mkuu kukutana Agosti, 4.
Chadema imeungana na CUF kutangaza ratiba ya
kuwapata wanachama watakaowania uongozi katika Uchaguzi Mkuu ambao
kikatiba unatakiwa ufanyike wiki ya mwisho ya Oktoba na kubakiza
mchakato wa kumpata mgombea mmoja kila nafasi ya uongozi.
Akielezea zaidi yaliyojiri katika vikao vya
kawaida vilivyofanyika Mei 3 na 4 mwaka huu, Mbowe alisema Kamati Kuu
ilipokea na kujadili makubaliano yaliyofikiwa ndani ya Ukawa.
Mbowe, ambaye pia ni mbunge wa Hai, alisema kuwa
kamati hiyo iliwapongeza viongozi hao kwa hatua walizofikia na kuwataka
wamalize masuala machache yaliyosalia ili wawajulishe Watanzania
wanaounga mkono umoja huo wajue kinachoendelea.
Post a Comment